MKEMIA MKUU WA SERIKALI AWATAKA WAKAGUZI KUONGEZA UFANISI
Mkemia Mkuu wa Serikali, Dkt. Fidelice Mafumiko, amewataka Wakaguzi wa Kemikali na Maabara za Kemia kuongeza ufanisi katika utekelezaji wa majukumu yao kwa lengo la kuleta tija na kuongeza mapato kwa Mamlaka.
Mkemia Mkuu wa Serikali, ameyasema hayo Juni 9, 2024 wakati akifunga kikao kazi cha mwaka cha Wakaguzi wa Kemikali na Maabara ya Kemia kilichofanyika katika Ofisi za Makao Makuu ya Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali jijini Dodoma.
“Tunapaswa kuzidisha juhudi ya kuongeza vyanzo vya mapato ili kuweza kuleta ufanisi katika utekelezaji wa majukumu yetu. Tunapaswa kutambua huu ni wajibu wetu na tusipotekeleza sisi hakuna atakayeweza kutekeleza. Maazimio yote tuliyokubaliana katika kikao hiki tukayafanyie kazi na kuyawekea mkakati wa kuyatekeleza na nani anatekeleza ili isije kuwa na mshangao tutakapokuja kukutana tena kwenye kikao kijacho.
Tutaangalia namna bajeti itakavyokuwa ili ikiwezekana vikao hivi kufanyika mara mbili kwa mwaka badala ya mara moja. Naamini kamati kwa kushirikiana na wataalam wa fedha tunaweza kufanikisha hili katika mwaka wa fedha 2024/2025 ingawa bajeti imeshapitishwa, kupanga ni kuchagua naamini inawezekana” alisema Dkt. Mafumiko.
Aidha, amezipongeza ofisi za Kanda kwa kujitahidi kukusanya mapato hali iliyopelekea kuwa zaidi ya asilimia sabini kwa baadhi ya Kanda huku Kanda ya Mashariki ikiwa kwenye asilimia tisini na moja, hali iliyopelekea kuanza kutoa tuzo kwa baadhi ya Wakaguzi waliofanya vizuri zaidi kwenye maeneo yao ya kazi.
“Mawasilisho yaliyowasilishwa na Meneja wa Kanda yameonesha kuleta mafanikio katika ukusanyaji wa mapato kwa sababu hakuna sehemu ambayo tuko chini ya asilimia 70. Hatua hii tuliyofikia tunapaswa kujipongeza kwa sababu wote tumechangia na tunapaswa kuendelea kuongeza nguvu zaidi ili kufikia malengo tunayojiwekea. Kupitia mkutano huu tutatoa zawadi kwa wakaguzi na waratibu wa ukaguzi na usajili wa kanda na wa Makao Makuu. Kwa kuanza tutaanza na hizi mbili na Utaratibu huu utakuwa unafanyika kila mwaka ikiwa ni sehemu ya kuwapa motisha ya utendaji kazi kwa wakaguzi wa Mamlaka. Katika mwaka ujao tutaanza kutoa zawadi hizi kwa Ofisi za Kanda ambazo zimefanya vizuri zaidi katika utekelezaji wa majukumu yake” alimaliza Mkemia Mkuu wa Serikali.
Akiongea baada ya kupokea tuzo ya Mkaguzi bora zaidi kutoka Ofisi ya Kanda ya Kati, Revocatus Mwamba, ameshukuru kwa kupokea tuzo hiyo na anaamini itamfanya kuongeza juhudi zaidi katika utekelezaji wa majukumu.
“Kwanza namshukuru sana Mkemia Mkuu wa Serikali kwa kuweza kutoa tuzo hizi, binafsi sikutarajia kama kuna kitu kama hiki kwa sababu huwa natekeleza majukumu yangu kwa kuzingatia Sheria, Kanuni na Taratibu kama mtumishi wa Umma. Kumbe tunapofanya hivyo kuna watu wengine wanatuangalia na kuona kile tunachokifanya kwa namna nyingine inatia moyo sana. Tuzo hii kwangu imeongeza hali zaidi katika kutekeleza wa majukumu yangu na inanifanya kujituma katika kazi na nawasihi watumishi wenzagu kutambua kwamba tunapotekeleza kazi zetu kuna watu wanatuangalia na kutupima” alisema Mwamba.