RAIS SAMIA AITAKA GCLA KUENDELEA KUTOA ELIMU KWA WACHIMBAJI MADINI
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, ameitaka Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali kuendelea kutoa elimu ya matumizi sahihi ya kemikali kwa wadau wote wanaojihusisha na shughuli za uchimbaji wa madini ili kulinda afya za Watanzania na Mazingira.
Dkt. Samia ameyasema hayo Oktoba 13, 2024 wakati akifunga Maonesho ya Saba ya Teknolojia ya Madini kitaifa yaliyofanyika katika viwanja vya Bombambili mkoani Geita.
Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan amesema elimu iendelee kutolewa zaidi kwani Kemikeli za mgodini zisipotumika kwa utaratibu wachimbaji watajikuta wanaelekeza gharama kubwa kwenye matibabu badala ya maendeleo.
“Tunawajibika kutoa elimu kwa wachimbaji na kusimamia kikamilifu sheria za nchi, Kemikali za migodini tusipozitumia kwa kuzingatia taratibu tutajikuta tunaelekeza gharama kubwa kutibu wananchi badala ya kujikita katika shughuli za Maendeleo” alisema.
Katika hatua Nyingine Dkt.Samia ameyataka mashirika mbalimbali yanayoshiriki katika maonesho hayo kujenga mabanda ya kudumu kwa kufuata ramani ambayo itatolewa na Serikali kupitia ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Geita.
Kwa upande wake Mkemia Mkuu wa Serikali, Dkt. Fidelice Mafumiko, amesema amepokea maelekezo ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa utekelezaji.