SIMAMIENI UBORA WA MAJI TIBA ILI KUWALINDA WAGONJWA WA FIGO
Watalaamu na Wachunguzi wa Maji Tiba wa Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali (GCLA), wametakiwa kuhakikisha wanasimamia na kujali ubora wa maji tiba wanayoyachunguza ili kulinda afya za wagonjwa wa figo wanaotegemea maji hayo katika Matibabu.
Wito huo umetolewa na Makamu wa Rais wa Chama cha Watalaamu wa Figo nchini, Profesa Paschal Ruggajo, wakati wa mafunzo kwa wachunguzi wa maji tiba yaliyofanyika katika Ukumbi wa Mkemia, jijini Dar es Salaam.
Profesa Ruggajo amesema takribani asilimia 90 ya maji tiba yanatumika katika matibabu ya wagonjwa figo, hivyo yasipolindwa na kusimamiwa ubora wake kisawasawa yanaweza kumletea shida mgonjwa wa figo na hata kuhatarisha uhai wake.
“kujali ubora wa maji tiba ni muhimu sana, ni wajibu wetu kama wasimamizi kuhakikisha tunasimamia kila kitu kinachohusiana na maji hayo kwani yasipolindwa na kutumika bila kuhakikisha usalama wake basi tutaleta shida kubwa kwa wagonjwa wengi wa figo ambao wanategemea maji haya katika matibabu yao.” alisema Profesa Ruggajo
Akizungumza kwa niaba ya Mkemia Mkuu wa Serikali wakati wa ufunguzi wa mafunzo hayo, Mkurugenzi wa Huduma za Sayansi Jinai, David Elias, amesema Mamlaka imepewa jukumu kusimamia na kuchunguza ubora wa maji tiba, hivyo watahakikisha wanasimamia kikamilifu uchunguzi wa sampuli za maji tiba zinazowasilishwa katika Mamlaka hiyo ili kuhakikisha wanalinda afya za wagonjwa watakaoenda kutumia maji hayo.
Naye Kaimu Mkurugenzi wa Uchunguzi wa Bidhaa na Mazingira, Dkt. Shimo Peter, amesema lengo la mafunzo hayo ni kuwajengea uwezo wachunguzi wa maji tiba ili kuhakikisha wanasimamia kikamilifu uchunguzi wa sampuli zinazohusiana na maji tiba na kuhakikisha zinafanyiwa kazi kikamilifu ili kutoleta shida kwa watumiaji wa maji hayo kitatibu.