TOENI HUDUMA KWA WATEJA KWA KUZINGATIA WELEDI
Wakaguzi wa kemikali na Maabara za Kemia wametakiwa kutoa huduma bora na zinazokidhi matarajio ya wananchi kwa wakati na kuhakikisha wanatumia lugha zenye staha na unyenyekevu hali itakayopelekea kuepusha malalamiko kutoka kwa wateja na wadau wanaohudumiwa na Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali (GCLA).
Wito huo umetolewa Julai 10, 2024 jijini Dar es Salaam na Kaimu Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano na Uhusiano kwa Umma wa Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali, Sylvester Omary, wakati wa mafunzo ya wakaguzi wa kemikali yanayofanyika katika Ofisi ndogo za Bunge jijini Dar es Salaam.
“Wadau wengi wamekuwa wakijivunia huduma zinazotolewa na Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali, mkifanya vibaya mtaharibu taswira nzima ya Mamlaka hii. Kila mmoja anapaswa kutambua huduma anayotoa kwa mteja wa ndani au wa nje anafanya hivyo kwa niaba ya Mamlaka, hivyo unatakiwa kuonesha ukarimu, unyenyekevu na weledi unapotoa huduma kwa mteja ili kutimiza lengo la utoaji huduma bora na inayomjali mteja kwa sababu tupo kwa ajili yao" alisema Sylvester.
Mafunzo hayo yamehusisha wakaguzi 29 wa Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali, wakitoka Makao Makuu na katika Ofisi za Kanda zinazosimamiwa na Mamlaka na yamefanyika kwa muda wa siku tano yakihusisha mada mbalimbali zinazohusiana na Usimamizi na Udhibiti wa masuala yanayohusiana na kemikali nchini.