UTOAJI WA ELIMU YA KEMIKALI KWA WADAU NI TAKWA LA KISHERIA
Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali (GCLA), kupitia Ofisi ya Kanda ya Kati - Dodoma imetoa mafunzo kwa wasimamizi wa kemikali kwa lengo la kuhakikisha wanawasimamia vyema shughuli mbalimbali za kemikali katika maeneo yao ya kazi.
Akizungumza wakati akifungua mafunzo hayo jijini Dodoma leo, Mkurugenzi wa Huduma za Udhibiti, Daniel Ndiyo, ameeleza kuwa dhumuni la kutoa mafunzo hayo ni kutokana na matakwa ya Sheria ya Kemikali ya Viwandani na Majumbani Sura 182, ambayo inataka wadau wote wanaojishughulisha na kemikali kuwa na uelewa wa matumizi sahihi na salama ya kemikali.
"Matumizi ya kemikali huzalisha kemikali taka ambazo zinaweza kuleta madhara kwa afya na mazingira zisipodhibitiwa, hivyo mafunzo haya ni muhimu katika kujenga uelewa wa kujihusisha na kemikali pamoja na kuzuia ajali zinazoweza kutokea kutokana na matumizi yasiyo sahihi na salama ya kemikali,” alisema Ndiyo.
Aidha, Mkurugenzi ameongeza kuwa mafunzo hayo yatawajengea uwezo wasimamizi wa kemikali katika kujua madhara na faida ya kemikali na wote wanatakiwa kujua namna sahihi ya kutumia kemikali na kushughulikia kemikali-taka zinazozalishwa kwani ajali mbalimbali za kemikali hutokana na sababu kadhaa, zikiwemo uelewa mdogo wa sheria za nchi na ufinyu wa rasilimali watu, hivyo kuchangia matumizi ya kemikali yasiyo sahihi na udhibiti hafifu wa kemikali taka.
Naye, Meneja wa Ofisi ya Kanda ya Kati – Dodoma, Gerald Meliyo, ametoa rai kwa wasimamizi wa kemikali kuhakikisha wanakuwa kwenye nafasi chanya ya kuwaelimisha wafanyakazi waliopo chini yao na pia kuwa mabalozi wa kuhamasisha wadau wengine kupata mafunzo pamoja na kueneza elimu ya matumizi salama ya kemikali katika maeneo yao ya kazi na nje ili kulinda afya za watu, wanyama na mazingira.
Kwa upande wake mshiriki wa mafunzo Mhandisi. Aron Mwaigaga, ameishauri Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali, kuendela kutoa elimu kwa wadau na wananchi kwa kuwaalika lakini pia kuwafikia katika maeneo yao ya kazi kwani elimu itawafikia wengi zaidi kutokana na maeneo ya kazi kuwa na wahusika wengi kwa wakati mmoja.
Mafunzo hayo ya usimamizi salama wa kemikali yanahusisha washiriki zaidi ya 80 kutoka mikoa ya Iringa, Tabora, Singida, Dodoma na Morogoro yatafanyika kwa siku tatu kuanzia Januari 24 hadi 26, 2024, jijini Dodoma.