Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

MAMLAKA YA MAABARA YA MKEMIA MKUU WA SERIKALI

GCLA Logo
ISO 9001:2015 Certified

WACHIMBAJI WAASWA KUZINGATIA MATUMIZI SALAMA YA KEMIKALI

Imewekwa: 09 Oct, 2024
WACHIMBAJI WAASWA KUZINGATIA MATUMIZI SALAMA YA KEMIKALI

Mkurugenzi wa Huduma za Udhibiti wa Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali, Daniel Ndiyo amewataka wachimbaji wakubwa na wadogo kuzingatia matumizi sahihi ya kemikali katika shughuli zao za kila siku ili kulinda Afya za viumbe hai na Mazingira.

Daniel Ndiyo, amesema hayo Oktoba 7, 2024 mkoani Geita kwenye maonesho ya 7 ya uwekezaji wa madini yanayofanyika katika viwanja vya Bombambili Geita.

“Jambo la msingi ni kuzingatia matumizi sahihi ya kemikali kwani shughuli za uchimbaji wa madini zinatumia kemikali katika hatua zote, kwa ufupi unapokuwa unalipua miamba ili upate mwamba wenye dhahabu unatumia kemikali inayochanganywa na vitu vingine ili upate vilipuzi vya kulipua mwamba na kemikali ni hatari kwani ni sumu” alisema

Katika hatua nyingine Mkurugenzi Ndiyo amewakumbusha wadau kuwa kuna juhudi za kuondosha matumizi ya Zebaki kwa miaka 10 ijayo hivyo kwa kipindi ambacho kemikali hii inatumika ni muhimu kuzingatia miongozo yote ya matumizi salama ya kemikali hiyo ili watumiaji, mazingira na wanyama wabaki salama

“Serikali imeingia mikataba ya kimataifa ya kupiga marufuku matumizi ya kemikali ya Zebaki hivyo ndani ya miaka 10 kemikali hii huenda isiendelee kutumika tena kutokana na madhara makubwa inayosababisha ikiwemo afya ya akili”

Kwa upande wake, Mateso Abel, ambaye ni mchimbaji mdogo wa madini amesema amejifunza madhara ya kemikali ya Zebaki ambayo amekuwa akiishika kwa mkono kwenye uchenjuaji wa dhahabu, hivyo atatumia vifaa kinga ili kuepuka madhara makubwa yanayoweza kujitokeza ikiwemo ugonjwa wa Saratani.