Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

MAMLAKA YA MAABARA YA MKEMIA MKUU WA SERIKALI

GCLA Logo
ISO 9001:2015 Certified

WADAU WATAKIWA KUZINGATIA MWONGOZO WA KEMIKALI YA AMMONIUM NITRATE

Imewekwa: 25 Aug, 2024
WADAU WATAKIWA KUZINGATIA MWONGOZO WA KEMIKALI YA AMMONIUM NITRATE

Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali kwa kushirikiana na wadau wanaohusika na uingizaji, uhifadhi, usafirishaji na utumiaji wa kemikali kutoka sekta binafsi pamoja na Mamlaka za Udhibiti ndani ya Serikali, wameandaa Mwongozo wa Usimamizi wa Kemikali ya Ammonium Nitrate.

Akizungumza katika uzinduzi wa Mwongozo huo uliofanyika katika ukumbi wa Ofisi ndogo ya Bunge jijini Dar es Salaam, Agosti 24, 2024, Mkemia Mkuu wa Serikali, Dkt. Fidelice Mafumiko, amesema kuwa Serikali ilitunga sheria ya Usimamizi na Udhibiti wa Kemikali za Viwandani na Majumbani Na.3 ya Mwaka 2003 ambayo inampa Mamlaka Msajili wa Kemikali za Viwandani na Majumbani kutengeneza miongozo mbalimbali ya usimamizi na udhibiti wa kemikali nchini pale atakapoona inafaa.

“Kutokana na umuhimu wa kemikali ya Ammonium Nitrate katika uchumi wa nchi, sambamba na madhara yake, Msajili wa kemikali kwa kushirikiana na wadau wa Serikali na sekta binafsi, ameandaa mwongozo utakaotumika katika hatua zote zinahusiana na kemikali hii. Mwongozo huu umeandaliwa kama sehemu ya juhudi zinazoendelea za kuboresha usimamizi na udhibiti wa kemikali nchini,” alisema Dkt. Mafumiko.

Aidha, Mkemia Mkuu wa Serikali amewataka wadau kutimiza wajibu wao kwa kuzingatia mwongozo huo unaohusiana na suala zima la kemikali ya Ammonium Nitrate ili kupunguza au kuondoa kabisa uwezekano wa ajali au madhara yatokanayo na kemikali hiyo.

“Mwongozo huu hautakuwa na maana yoyote endapo hautafuatwa au kuzingatiwa kikamilifu wakati tutakapokuwa tunajishughulisha na kemikali hii. Ninapenda kuwaasa kila mmoja wetu ahakikishe anautekeleza ipasavyo. Nawahakikishia kuwa, sisi kwa upande wa usimamizi na udhibiti tutafanya sehemu yetu ipasavyo,” alisisitiza Dkt. Mafumiko.

Kwa upande wake Makamu wa Rais wa Chama cha Mawakala wa Forodha Tanzania, Waheed Saudin, ameipongeza Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali kwa uzinduzi wa Mwongozo wa Usimamizi wa Kemikali ya Ammonium Nitrate kwani Ammonium Nitrate ni kemikali ambayo isiposimamiwa vizuri ni hatari kwa afya ya binadamu, mazingira na taifa kwa ujumla.

“Kupitia mwongozo huu tumeelekezwa jinsi gani ya kuweza kupokea hiii kemikali ya Ammonium Nitrate, kuhifadhi, kusafirisha na kutumia kemikali hii kwa kuhakikisha tunazingatia usalama wetu binafsi na mazingira ili kuepusha athari,” alisema Waheed.