Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

MAMLAKA YA MAABARA YA MKEMIA MKUU WA SERIKALI

GCLA Logo
ISO 9001:2015 Certified

WAKULIMA WASHAURIWA KUPATA ELIMU SAHIHI YA KEMIKALI

Imewekwa: 08 Aug, 2024
WAKULIMA WASHAURIWA KUPATA ELIMU SAHIHI YA KEMIKALI

Wakulima kote nchini wameshauriwa kujitokeza kwa wingi kutembelea banda la Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali ili waweze kupata elimu kuhusu majukumu mbalimbali yanayofanyika katika Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali ikiwemo matumizi sahihi ya kemikali pamoja na uchunguzi wa kimaabara wa mazao.

Akizungumza jijini Dodoma katika maonesho ya Nane nane ambayo kitaifa yamefanyika katika viwanja vya Nzuguni, Dodoma, Meneja wa Kanda ya Kati, Gerald Meliyo, amesema mkulima anapopata elimu kuhusiana na masuala ya kilimo itamsaidia kulima kilimo bora na chenye tija na ataepukana na athari mbalimbali anazokumbana nazo shambani.

“Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali inafanya uchunguzi wa mazao mbalimbali ili kuweza kuona kama mazao hayo yanafaa kwa matumizi pia tunatoa elimu kuhusu matumizi sahihi ya kemikali,hivyo tunawakaribisha sana wakulima kwenye banda la Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali ili waweze kupata elimu kuhusiana na shughuli mbalimbali za Mkemia, ambapo kuna usajiri wa kemikali za aina mbalimbali, tunasajiri wadau wanaojihusisha na kemikali za viwandani na majumbani ili kuhakikisha kwamba kemikali zinazoingia nchini zinakuwa bora na sahihi kwa matumizi ya nchi kwa mujibu wa sheria” alisema Meliyo.

Kwa upande wake Kaimu Mkurugenzi wa Uchunguzi wa Bidhaa na Mazingira, Dkt. Shimo Peter, ameongeza kuwa mkulima anapopata elimu sahihi ya matumizi salama ya kemikali ataweza kulinda afya zao pamoja na mazingira na kutoathiri maisha na familia zao.

“Tunawaasa wakulima na wajasiriamali wanaotumia kemikali kufika katika Mabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali kupata elimu ya matumizi sahihi ya kemikali ili waweze kulinda afya zao, lakini pia waweze kuongeza kipato cha familia na Taifa kwa ujumla” alisema Dkt Shimo.