Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

MAMLAKA YA MAABARA YA MKEMIA MKUU WA SERIKALI

GCLA Logo
ISO 9001:2015 Certified

WANANCHI WASHAURIWA KUEPUKA KULALA NA JIKO LA MKAA

Imewekwa: 22 Feb, 2024
WANANCHI WASHAURIWA KUEPUKA KULALA NA JIKO LA MKAA

Mganga Mkuu wa Manispaa ya Iringa, Dkt. Godfrey Mbangali, amewataka viongozi wa Serikali za Mitaa, Watoa elimu ya Afya kwa Jamii na Maafisa Afya Mazingira ngazi ya Kata kutoa elimu kwa jamii kuhusu matukio ya sumu ili kulinda afya ya jamii na kupunguza vifo vitokanavyo na madhara ya sumu.

Dkt. Mbangali aliyasema hayo wakati akifungua mafunzo ya kudhibiti matukio ya sumu kwa Wenyeviti wa Mitaa, Afisa Afya na Mazingira pamoja na Wahudumu wa Afya ya ngazi ya Jamii, yaliyotolewa na Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali kupitia Kitengo cha Kudhibiti Matukio ya Sumu yaliyofanyika mjini Iringa.

“Niwasihi washiriki wa mafunzo haya mkawe mabalozi katika kupunguza na kudhibiti matukio ya sumu katika maeneo yenu ya kazi, jamii inayowazunguka na sehemu zingine yatakapotokea matukio ya sumu. Tuhakikishe tunakuwa tayari muda wote, kwani matukio ya sumu ni matukio ya dharura, hivyo utayari wenu wa utoaji huduma au taarifa kwa aliyepatwa na tukio la sumu utasaidia upatikanaji wa huduma stahiki kwa mhanga”, alisema Dkt. Mbangali.

Aidha, Mganga Mkuu amewataka washiriki wa mafunzo hayo kuwa katika nafasi nzuri ya kusambaza elimu kuhusu masuala mbalimbali ya sumu kwa jamii inayowazunguka na pia kushirikiana na Kituo cha Taifa cah Kudhibiti Matukio ya Sumu hususani sumu ya carbon monoxide.

Kwa upande wake Msimamizi wa Kituo cha Taifa cha Kudhibiti Matukio ya Sumu kutoka Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali, Yohana Goshashy amewataka wananchi kujilinda na kuchukua tahadhari dhidi ya matukio ya sumu hasa sumu ya carbon monoxide inayotengenezwa na mkaa usioungua na kuisha. Hivyo, ameshauri kuepuka kulala chumbani na jiko la mkaa lenye moto na pia kujenga nyumba yenye sehemu mbalimbali za kupitisha hewa.

Naye, Muhudumu wa Afya Kata ya kwa Kilosa, Khadija Mili ameishukuru Mamlaka kwa kutoa elimu ya sumu Manispaa ya Iringa na kusema kuwa masuala ya sumu yanaepukika hivyo, wapo tayari kueneza elimu ya kudhibiti matukio ya sumu kwa jamii wanayoihudumia