Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

MAMLAKA YA MAABARA YA MKEMIA MKUU WA SERIKALI

GCLA Logo
ISO 9001:2015 Certified

WASIMAMIZI WA KEMIKALI ZINGATIENI MATUMIZI SALAMA YA KEMIKALI

Imewekwa: 17 Dec, 2024
WASIMAMIZI WA KEMIKALI ZINGATIENI MATUMIZI SALAMA YA KEMIKALI

Wasimamizi wa kemikali kutoka Makampuni, Taasisi na mashirika mbalimbali yanayojihusisha na matumizi ya kemikali, wametakiwa kuzingatia matumizi sahihi ya kemikali hizo ili kuepusha kuchepushwa na kutumika kinyume na matumizi yaliyolengwa ikiwemo kutumika kutengeneza dawa za kulevya.

Akizungumza wakati wa ufunguzi wa mafunzo kwa wasimamizi hao yaliyofanyika Jijini Arusha katika Hoteli ya Mount Meru, kwa niaba ya Mkurugenzi wa Huduma za Udhibiti wa Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali, Magreth Mtenga, amesema ni jukumu la kila mmoja kuhakikisha anazingatia sheria ya Udhibiti na usimamizi wa matumizi ya kemikali.

“Serikali imekuwa ikitumia njia mbalimbali ili kuongeza jitihada ikiwemo kutunga sheria kwa lengo la kupambana na kudhibiti uchepushwaji wa kemikali hususani bashirifu ambazo endapo zisipodhibitiwa vizuri zinaweza kutumika katika kutengeneza dawa za kulevya na hata nyingine kutumika kutengeneza silaha” amesema Mtenga.

Kwa upande wake Kamishna kutoka Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya, Dominician Domician, amesema kuwa baadhi ya wadau wanaojihusisha na  kemikali wamekuwa si waaminifu na kuchepusha kemikali bashirifu ambazo  nyingine zimekuwa zikitumika kutengenezea dawa za kulevya.

“Kwa kweli niwasii sana nyie kama wasimamizi wa kemikali, mjitahdi kuwa wazalendo na kuzingatia sheria zinazosimamia matumizi ya kemikali, simamieni watu wenu vizuri wasichepushe kemikali bashirifu kwenda kutumika kwa matumizi mengine, kwani ni hatari katika mazingira ya matumizi ya dawa za kulevya.” Alisema Dominic.

Naye Meneja wa Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali Kanda ya Kaskazini, Eliamini Mkenga, amesema wadau wote wa kemikali lazima wawe wamesajiliwa kwa mujibu wa sheria ili waweze kufanya biashara zao kwa usalama ili kulinda afya za binadamu na Mazingira.

Mafunzo hayo  ya siku tatu  yamehusisha mada mbalimbali kutoka kwa wataalam wa mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali, ambapo  wasimamizi wa kemikali kutoka Makampuni, Taasisi na Mashirika mbalimbali zaidi ya 45 wameweza kushiriki katika mafunzo hayo.