Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

MAMLAKA YA MAABARA YA MKEMIA MKUU WA SERIKALI

GCLA Logo
ISO 9001:2015 Certified

WASIMAMIZI WA SAMPULI ZA MAKOSA YA JINAI WANOLEWA

Imewekwa: 17 Dec, 2024
WASIMAMIZI WA SAMPULI ZA MAKOSA YA JINAI WANOLEWA

Wasimamizi wa Sampuli za Makosa ya Jinai wakiwemo Maafisa wa Jeshi la Polisi, Maafisa Ustawi wa Jamii, Madaktari na Wataalam wa Maabara wamepewa mafunzo ya usimamizi wa sampuli za makosa ya jinai na Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali kupitia Ofisi ya Kanda ya Kusini.

Akizungumza wakati wa kufungua mafunzo hayo yaliyofanyika mjini Songea mkoani Ruvuma Desemba 16, 2024, Mkuu wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai Mkoa wa Ruvuma, Charles Makunja, amewataka wadau wa haki jinai kuhakikisha mnyonyoro wa Haki Jinai kuhakikisha wanatekeleza majukumu yao kwa weledi na pia kuhakikisha haki inapatikana kwa wakati kama ilivyo nia ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan.

“Kama wadau ambao tunahusika katika uchukuaji wa sampuli au vielelezo na kuviwasilisha Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali kwa uchunguzi wa kisayansi, nawaasa washiriki mzingatie yatakayofundishwa ili kuweza kuzidisha umahiri katika utendaji kazi wenu,” alisema Makunja.

Pia, Makunja amewataka wadau hao wa haki jinai kuwa mabalozi na kuhakikisha wanawapa elimu wataalam wengine ambao hawajapata nafasi ya kushiriki mafunzo hayo ili kwa pamoja kuongeza ufanisi katika majukumu yao.

Kwa upande wake Meneja wa Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali, Ofisi ya Kanda ya Kusini, Hadija Mwema amewapongeza Wakuu wa Upelelezi Wilaya za Ruvuma, Wakurugenzi na Waganga Wakuu wa Hospitali kwa kuruhusu watumishi wao kushiriki mafunzo hayo kwani yanaendelea kujenga na kuimarisha ushirikiano uliyopo kati ya Mamlaka na Wadau wa Haki Jinai.

Naye, Mkuu wa Upelelezi Wilaya ya Songea, Juma Baltazar ameipongeza Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali kwa kusogeza huduma za Mamlaka wilayani humo kwani kwa sasa wanatekeleza majukumu yao yanaohusiana na masuala ya haki jinai kwa wakati.

“Kwa sasa tunawasilisha vielelezo vya makosa ya jinai kwa wakati Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali kwa ajili ya uchunguzi wa kisayansi tofauti na hapo awali ambapo tulilazimika kusafirisha vielelezo au sampuli Mtwara kwa ajili ya uchunguzi,” alimaliza Baltazar.