Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

MAMLAKA YA MAABARA YA MKEMIA MKUU WA SERIKALI

GCLA Logo
ISO 9001:2015 Certified

WATUMISHI WA MAMLAKA WATAKIWA KUWA WABUNIFU

Imewekwa: 03 May, 2024
WATUMISHI WA MAMLAKA WATAKIWA KUWA WABUNIFU

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Philip Mpango amewapongeza wafanyakazi nchini kwa kuadhimisha Sikukuu ya Wafanyakazi Duniani.

Mhe. Mpango alitoa pongezi hizo wakati wa Sherehe za Maadhimisho ya Siku ya Wafanyakazi Duniani (Mei Mosi), yaliyofanyika kitaifa katika uwanja wa Sheikh Amri Abeid Karume jijini Arusha Mei 1, 2024.

“Niwashukuru kwa mchango wenu adhimu katika ujenzi wa Taifa letu. Kama yalivyo makundi mengine kwenye jamii, kundi la wafanyakazi lina mchango mkubwa sana katika ujenzi wa nchi yetu. Serikali itaendelea kuimarisha mazingira ya kazi ikiwemo kuboresha maslahi ya wafanyakazi kadri hali ya uchumi itakavyoruhusu,” alisema Dkt. Mpango.

Aidha, Makamu wa Rais ametoa wito kwa wafanyakazi, kuendelea kutekeleza majukumu yao kwa bidii, maarifa, uadilifu na kwa moyo wote, huku akiwataka kutanguliza maslahi ya Taifa mbele na kuendelea kuongeza tija katika utendaji kazi. Pia, amevisihi vyama vya wafanyakazi kushirikiana na Serikali na Waajiri kuhakikisha wanaongeza tija kwenye maeneo yao ya kazi kwa manufaa ya Taifa na wafanyakazi wenyewe, sambamba na kupaza sauti kuhusu madai ya wafanyakazi.

Kwa upande wake Meneja wa Mamlaka Ofisi ya Kanda ya Kaskazini, Eliamini Mkenga amewataka watumishi wa Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali kuwa wabunifu katika utendaji kazi na pia amewashukuru watumishi wa Mamlaka kutoka kanda mbalimbali kuungana na wafanyakazi wote nchini kuadhimisha Siku ya Wafanyakazi Duniani.

Jackson Mwijage ambaye amekuwa Mtumishi Bora wa mwaka kutoka Mamlaka, amemshukuru Mkemia Mkuu wa Serikali, Dkt. Fidelice Mafumiko kwa kuwezesha watumishi kufanya kazi katika mazingira rafiki pamoja na kuwahamasisha watumishi kuendelea kufanya kazi kwa weledi ili kufikia malengo ya Mamlaka. Pia, Mwijage amewasihi watumishi kuendelea kufanya kazi kwa umoja, mshikamano, upendo na kuendelea kujituma huku wakimtanguliza Mungu.