Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

MAMLAKA YA MAABARA YA MKEMIA MKUU WA SERIKALI

GCLA Logo
ISO 9001:2015 Certified

WAZIRI MKUU AIPONGEZA MAMLAKA KWA UTOAJI HUDUMA BORA KWA JAMII

Imewekwa: 05 Jul, 2024
WAZIRI MKUU AIPONGEZA MAMLAKA KWA UTOAJI HUDUMA BORA KWA JAMII

Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Kassim Majaliwa ameipongeza Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali kwa namna inavyoendelea kutoa huduma bora na nzuri kwa jamii.

Waziri Mkuu Majaliwa ametoa pongezi hizo jijini Dodoma wakati alipotembelea banda la Mamlaka katika maonesho ya Wiki ya Madini yaliyofanyika katika ukumbi wa Jakaya Kikwete, jijini Dodoma.

“Sisi hatuna mashaka na Taasisi ya Mkemia Mkuu wa Serikali, mnafanya kazi nzuri sana ya kuhudumia wananchi, sasa muwahudumie pia na watu wa madini ili kutambua aina ya kemikali zipi nzuri na zipi hazifai kutumika. Kwa hiyo endeleeni kubainisha hayo ili jamii ifanye kazi ya uchimbaji bora” alisema Waziri Mkuu Majaliwa.

Kwa upade wake Katibu Mkuu Wizara ya Madini, Kheri Mahimbali ameishauri Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali kufanya kikao cha pamoja na STAMICO na Wizara ya Madini kutengeneza mwongozo utakaosaidia wachimbaji wa madini kujua kiasi cha madini kilichopo ardhini kabla ya kuanza kuchimba.

“Sasa mjaribu kukutana mfanye kikao cha pamoja kati yenu, STAMICO na Wizara ya Madini, tengenezeni mwongozo ili uwasaidie wachimbaji wa madini kujua kiasi cha madini kilichopo ardhini kabla hawajaanza kuchimba nadhani hii itakuwa mbinu yenye tija kwa wachimbaji” alisema Mahimbali.

Katika hatua nyingine, wakati akifunga maonesho hayo waziri Mkuu Mh.Kassim Majaliwa ameitaka wizara ya madini kuhakikisha inashirikiana na wadau mbalimbali wa ndani na nje ya nchi ili kupata ufumbuzi wa matumizi ya teknolojia zitakazotumika kuongeza thamani ya madini.

“Sasa nitoe rai kwa wizara ya madini endeleeni kushirikiana na wadau mbalimbali wa ndani na nje ya nchi katika kutatua na kutafuta ufumbuzi wa namna tutakavyotumia teknolojia za uongezaji thamani madini na kuwezesha madini yetu kutumika katika kuzalisha bidhaa mbalimbali, ambazo zinahitajika sana nchini na duniani kote kutokana na kuongezeka kwa mahitaji, pamoja na kuendelea kuongezeka kwa idadi ya watu duniani” alisema Waziri Mkuu Kassim Majaliwa.

Maonesho ya wiki ya madini yalifunguliwa rasmi Juni 20,2024 na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Philip Mpango na kufungwa Juni 27,2024 na Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa.