GCLA YAPELEKA TABASAMU KWA WATOTO MOI

Watumishi Wanawake wa Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali (GCLA) Machi 14, 2025, wametoa msaada wa mahitaji mbalimbali yenye thamani ya shilingi milioni 3.3 kwa watoto wenye changamoto ya vichwa vikubwa na mgongo wazi katika Taasisi ya Tiba ya Mifupa na Ubongo Muhimbili (MOI).
Akizungumza baada ya kukabidhi msaada huo, Mwenyekiti wa Wanawake wa GCLA, Veronica Chiligati, amesema kuwa msaada huo umetokana na upendo walionao wanawake wa Mamlaka na pia ni utamaduni wao kila kipindi cha Maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani kupeleka misaada kwa wahitaji mbalimbali.
“Tunawashukuru sana wote waliotuunga mkono, tunaomba tuendelee kuchangia zaidi kwa sababu waliokuja hospitali leo wameona hali halisi ya hawa wagonjwa waliopo hapa na wengi wamekaa muda mrefu na wana uhitaji sana hivyo, tunaomba tuendelee kutoa sadaka zaidi kuwasaidia wenzetu,” alisema Chiligati.
Aidha, mbali na msaada huo Mamlaka pai imechangia gharama ya shilingi milioni 1.4 kwa ajili ya matibabu ya upasuaji wa watoto 7 wenye vichwa vikubwa na mgongo wazi waliolazwa MOI.
Kwa upande wake Afisa Ustawi wa Jamii – MOI, Theresia Tarimo, amewashukuru watumishi wa Mamlaka kwa msaada waliotoa na kuwaomba kuendelea na moyo huo kwani Taasisi ya MOI inapokea wagonjwa ambao wanatoka katika matabaka tofauti tofauti wakiwemo wagonjwa wa ajali za boda boda ambao hawana ndugu, watoto wenye ulemavu ambao wametengwa na jamii.
“Napenda kutoa rai kwa jamii inayotuzunguka, tunawakaribisha sana katika Taasisi ya MOI ili waweze kuja kuungana nasi katika kutoa huduma bora kwa wagonjwa kwa kuangalia wagonjwa wenye uhitaji maalum kama ambao hawana uwezo ili kupunguzia taasisi gharama za matibabu,” aliongeza Theresia.
Aidha, katika vitu vilivyotolewa na Mamlaka ni pamoja na pempasi katoni 5, mchele wa uji kilo 75, maziwa ya kopo 12, sukari kilo 20, taulo za kufuta (wipes) katoni 3 na dawa za binadamu zenye thamani ya shilingi laki 8.