MWENYEKITI WA BODI AWAPONGEZA WATUMISHI WA KANDA YA ZIWA

Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali, Christopher Kadio, amewapongeza watumishi wa Mamlaka, Kanda ya Ziwa, kufuatia mrejesho mzuri alioupata kutoka wa wadau wa Mamlaka alipokuwa katika ziara ya kikazi katika mikoa ya Kanda ya Ziwa.
Mwenyekiti wa Bodi, Christopher Kadio amesema hayo Machi 11, 2025, wakati akiwaaga watumishi wa Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali, Ofisi ya kanda ya Ziwa baada ya kuhitimisha ziara yake ya kikazi.
“Tunawapongeza kwa kazi nzuri, tumetembelea wadau wengi na hatujakutana na changamoto yeyote zaidi ya pongezi kutoka kwa wadau ambao wameonesha kuridhishwa na utendaji kazi wenu. Kwa hiyo muendelee na kasi hiyo na niwaambie tu mlango uko wazi kwangu na kwa wajumbe wa bodi kwa jambo lolote ambalo unahisi ni la kujenga tuwasiliane kwa maslahi mapana ya Mamlaka na taifa letu” alisema Mwenyekiti wa Bodi.
Kwa upande wake Mjumbe wa Bodi, Doris Njelekela, amesema amejifunza mambo mengi na kusikiliza changamoto za wadau wa Mamlaka na kupata picha halisi ya aina ya wadau ambao Mamlaka inawahudumia
“Tumeweza kutembelea wadau wengi wakiwemo wachimbaji wakubwa na wadogo na wadau wengine wa kemikali na kiukweli tumejifunza mambo mengi na tumepata picha halisi ya aina ya watu tunaowahudumia, ili hata tukirudi katika vikao vya bodi vya maamuzi tutakuwa tunajua tunafanya maamuzi yanayowagusa wadau wa aina gani” alisema Njelekela.
Naye mjumbe wa Bodi, Mukabatunzi Rwakilomba alisema ziara hiyo imekuwa na manufaa makubwa kwani wamewafikia wadau wa migodi mbalimbali na wadau wa kemikali, vilipuzi pamoja na maabara.
“Ziara imekuwa na manufaa makubwa kwa sisi wajumbe wapya wa Bodi ya Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali, kwani imekuwa ni nafasi nzuri ya kujifunza na kujionea wadau tunaowahudumia, hali ambayo imetujengea picha ambayo itatusaidia kwenye kufanya maamuzi wakati wa vikao vya bodi” alisema Rwakilomba.