Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

MAMLAKA YA MAABARA YA MKEMIA MKUU WA SERIKALI

GCLA Logo
ISO 9001:2015 Certified

MAFUNZO YA USIMAMIZI WA SAMPULI ZA HAKI JINAI NI TIJA MTAMBUKA

Imewekwa: 17 Mar, 2025
MAFUNZO YA USIMAMIZI WA SAMPULI ZA HAKI JINAI NI TIJA MTAMBUKA

Mkufunzi Mkuu wa Chuo cha Taaluma ya Polisi Dar es Salaam, Kamishna Msaidizi wa Polisi, Andrea Legembo, Amesema kuwa mafunzo ya Usimamizi wa Sampuli za Jinai yanayotolewa na Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali kwa Maafisa wa Jeshi la Polisi yana tija kwa jeshi hilo kwa sababu Jeshi la Polisi ni miongoni mwa vyombo vya dola vinavyohusika na utoaji wa haki.

Kamishna Legembo amesema hayo alipokuwa akifunga mafunzo ya Usimamizi wa Sampuli za Jinai na Usimamizi na Udhibiti wa Kemikali kwa Maafisa wanafunzi wa Jeshi la Polisi yaliyofanyika katika Chuo cha Taaluma ya Polisi Dar es Salaam Machi 13, 2025.

“Ikiwa sisi Jeshi la Polisi tutafanya kazi zetu za uchukuaji wa vielelezo kwa weledi mkubwa kuanzia uchukuaji wa sampuli, ufungashaji na usafirishaji hadi Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali kwa uchunguzi, itawezesha majibu kutoka yakiwa sahihi na kwa wakati na hivyo tutakuwa tumetimiza wajibu wetu wa kutoa haki kwa wananchi wetu” alisema.

Kamisha Legembo, amebainisha kuwa, tija itakayopatikana kutokana na mafunzo hayo haitakuwa kwa Jeshi la Polisi pekee bali ni mtambuka kwa pande zote, kwa taasisi zinazoshirikiana na mnyororo wa haki jina kwa upande mmoja na mwananchi kwa upande mwingine.  Amefafanua kuwa Ofisi ya Mkemia Mkuu wa Serikali itafaidika kwa kurahisisha kazi zake za kutoa majibu sahihi na kwa wakati na kwa upande wa raia kupata majibu yao kwa wakati na hivyo kujenga imani kwa serikali kuwa imeweka usimamizi mzuri na uwajibikaji katika majukumu yake.

“Natoa wito kwa Maafisa wanafunzi wa Jeshi la Polisi kuwa mabalozi wazuri kwa kuwashirikisha wenzenu ambao bado hawajapata  mafunzo hayo ujuzi na maarifa mliyopata. Ujuzi mliopata mkautumie kwa weledi kwa manufaa yenu wenyewe, kwa jeshi la Polisi na kwa manufaa ya wananchi mnaokwenda kuwahudumia” alisema.

Aidha, alifafanua kuwa mafunzo hayo yatasaidia kuwa sehemu ya utekelezaji wa maboresho yaliyokuwa yameagizwa na Mhe. Rais wa Jamhuri wa Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, ya kuhakikisha kwamba haki inatolewa posipo kuwa na vikwazo wala ucheleweshwaji.

Kwa upande wake Meneja wa Ofisi ya Kanda ya Mashariki, ambaye alimwakilisha Mkemia Mkuu wa Serikali, Danstan Mkapa, alisema kuwa mafunzo hayo yamekuwa na tija kubwa kwa sababu kulikuwa na ubadilishanaji wa uzoefu kwa pande zote mbili. Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali imeweza kupata ushauri wa masuala mbalimbali kutoka kwa maafisa hao wanafunzi wa Jeshi la Polisi ambao kiuhalisia wengi wao wanafahamu majukumu ya Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali na wamekuwa wakishirikiana katika maeneo mengi.

“kuna vitu vingi wametushauri na sisi kama ofisi tumeyachukuwa, na mambo mengine wamechukua kutoka kwetu na hii yote ni katika kuboresha utekelezaji wa majukumu yetu katika haki jinai”, alisema.

Mafunzo ya Usimamizi wa Sampuli za Haki Jinai na Usimamizi na  Udhibiti wa kemikali yametolewa kwa Maafisa wanafunzi zaidi ya mia tisa (900) wa Chuo cha Taalum cha Jeshi la Polisi Kurasini, Dar es Salaam.