Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

MAMLAKA YA MAABARA YA MKEMIA MKUU WA SERIKALI

GCLA Logo
ISO 9001:2015 Certified

MKEMIA MKUU WA SERIKALI AIMIZA UADILIFU MAHALA PA KAZI

Imewekwa: 15 Dec, 2023
MKEMIA MKUU WA SERIKALI AIMIZA UADILIFU MAHALA PA KAZI

Mkemia Mkuu wa Serikali Dkt. Fidelice Mafumiko, amewataka Watumishi wa Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali, Ofisi ya Kanda ya Kaskazini – Arusha kufuata misingi, kanuni, taratibu na kufanya kazi kwa uadilifu na kuzingatia maadili ya utumishi wa umma ili kuongeza tija katika kuwahudumia wananchi.

Dkt. Mafumiko ametoa wito huo Disemba 8, 2023, wakati akifungua kikao maalum cha Uadilifu kwa Watumishi wa Mamlaka kilichofanyika katika Ofisi ya Kanda ya Kaskazini.

Dkt. Mafumiko amewataka watumishi wa Mamlaka kuzingatia uadilifu ili watekeleze majukumu waliokabidhiwa kama dhamana ya kuhudumia umma bila upendeleo na kuweka jitihada katika kuhakikisha watumishi wanajenga umahiri kwani kutaongeza fursa za maendeleo binafsi.

“Uadilifu ni uwezo wa mtumishi kutenda anayopaswa kutenda na kutotenda asiyopaswa kutenda kwa kujisimamia yeye mwenyewe. Mambo ambayo mtumishi hapaswi kuyatenda ni pamoja na kupokea rushwa, kuchelewa kufika kazini au kutofika kabisa kazini kwa visingizio vya uongo, kutoa huduma kwa upendeleo kwa wateja wa ndani na nje, kutomaliza kazi kwa wakati, kutoa taarifa za uongo, kujihusisha na mahusiano ya kimapenzi mahali pa kazi na mengine,” alisisitiza Dkt. Mafumiko.

Katika hatua nyingine Mkemia Mkuu wa Serikali ameridhia Kamati ya Uadilifu kuanzisha utaratibu wa kuwaelimisha watumishi wa Mamlaka ili kuendelea kuwajengea uwezo watumishi kuhusu masuala ya maadili.

Naye, Meneja wa Ofisi ya Kanda ya Kaskazini Eliamini Mkenga, ameishukuru Kamati ya Uadilifu kutoa mafunzo kwa watumishi wa Kanda hiyo, hivyo wategemee kuongezeka kwa uadilifu na umahiri wa hali ya juu kutoka kwa watumishi wa Kanda ya kaskazini katika utekelezaji wa majukumu yao. Vilevile Mkenga amewapongeza watumishi wa Kanda kwa weledi na utendaji kazi mzuri katika utekelezaji wa majukumu yao ambayo inachangia katika ukuaji wa taasisi.